"Safari ya Maarifa: Kuelimisha na Kusaidia Vijana Kupitia Blog Hii"
Rafiki yangu, nafurahi sana kukukaribisha kwenye blog hii! Leo ni siku ya kwanza kushirikiana nawe maarifa na uzoefu wangu, na ningependa kutumia fursa hii kueleza sababu kubwa iliyonisukuma kuanzisha safari hii ya kushirikisha elimu na maarifa.
Kwa zaidi ya miaka tisa (9), nimekuwa nikifanya kazi kwa ukaribu na watoto na vijana balehe. Katika safari hii, nimejifunza mambo mengi kupitia vijana na watoto niliowasaidia kusonga mbele katika maisha yao. Nilipata msukumo wa kuwasaidia vijana wenzangu baada ya mimi mwenyewe kukumbana na changamoto za balehe, lakini kwa msaada wa wataalamu wa vijana, nilipata mbinu sahihi za kukabiliana nazo.
Lengo langu ni kutumia ujuzi na uzoefu wangu kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya watoto na vijana balehe kwa kusaidia ukuaji na ustawi wao. Kupitia blog hii, nitashirikisha makala mbalimbali kuhusu makuzi na malezi ya watoto na vijana balehe ili kuwasaidia kupita kipindi hiki cha mpito kwa usalama.
Pia, tutapata nafasi ya kushirikishana uzoefu kama kijana au mlezi, tukijifunza kwa pamoja mbinu bora za kuwalea na kuwaelekeza vijana wetu.
Mwaka 2016, nilipata fursa ya kufanya kazi na shirika lisilo la kiserikali, Baylor Foundation Tanzania, lenye Dira ya kutoa huduma bora za afya kwa watoto na familia zinazoishi na VVU, kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya, na kufanya utafiti wa kiafya unaoendana na mahitaji ya jamii.
Katika nafasi yangu ya kazi na Baylor Foundation Tanzania, nilihusika katika kuboresha huduma kwa vijana balehe katika kliniki ya mfano ya Baylor-TZ na vituo vinavyosaidiwa. Nilishiriki katika programu za elimu rika, kuongeza ushiriki wa vijana katika utoaji wa huduma za afya, na kusaidia kudhibiti maambukizi ya VVU kwa vijana.
Majukumu yangu yalijumuisha
kuratibu na kusimamia programu kama vile Teen Club, mikutano ya viongozi wa
vijana, mafunzo ya waelimishaji rika, usimamizi wa Teen Club, kambi za
Jitambue, programu ya Timiza Lengo, na programu za Afya ya Uzazi kwa
Vijana (ASRH).
Sababu kubwa iliyonisukuma kuanzisha blog hii ni kuona jinsi vijana wengi wanavyokosa elimu sahihi kuhusu balehe na changamoto zake, hivyo kushindwa kuchukua hatua stahiki.
Karibu sana rafiki yangu!
Tutaendelea kujifunza kwa
pamoja kupitia makala zinazofuata. Nakutakia siku yenye mafanikio!
Comments
Post a Comment